SOKA IGIN

WE INSPIRE AND EMPOWER FOR CHRIST'S MISSION.

Ijumaa, 23 Machi 2018

SIFA 15 ZA MJASIRIAMALI



Zifuatazo ni sifa 15 za Mjasiriamali.

1. Ubunifu
Ubunifu ni kionjo cha muhimu sana katika Ujasiriamali.Kwa kwawaida mjasiriamali anapenda kuwa tofauti ili awashangaze watu.Anapenda kuwa mwanzilishi wa vitu au jambo.

2. Uwezo wa kubaini fursa katika Matatizo
Vijana walioko ktk mazingira hatarishi au chokoraa mjini Arusha walipokaa kikao kubuni mbinu ya kujikimu waligundua fursa ya kuosha vioo vya magari pale mianzini kwenye mataa (Trafic lights) na kwa kufanya hivyo kwa kujitolea wakawa wanapata fedha  nyingi
kutoka kwa madreva waliofurahi kuoshewa vioo vya magari yao tofauti na biashara yao ya awali ya kuombaomba. Hivyo hawa waliona tatizo la vioo vichafu vya magari ikawa ni fursa kwao ya kupatia ajira.

3. Kujituma na kujitolea
Fursa nyingi za kijasiriamali zilipatikana pale ambapo mtu alipoamua kujitolea na kujituma bure bila malipo yoyote; hii ni sifa ya Muhimu sana kwa mjasiriamali yeyote. .

4. Kuhitaji mafanikio
Mjasiriamali anaamini katika maendeleo na akilini mwake anajua anachokifanya kitamtoa katika hali aliyo nayo. Mara nyingi huyu mjasiriamali anapenda kuendelea kuwepo katika ramani ya mafanikio; hivyo njozi yake, wimbo  wake na maneno yake ni mafanikio.

5. Kuvumilia changamoto
Mjasiriamali kwa kawaida anakumbana na changamoto zinazotishia uchumi, familia na hata heshima yake pale anapoanza kufanya jambo au mradi. Hii ni sifa ya ujasiri ambayo inabeba neno ujasiriamali.
.
6. Uhuru
Uhuru ni kionjo kingine cha mjasiriamali kwani anaamini kuwa akifanya mambo yake bila kuingiliwa na mtu mwingine anaweza kufanikisha kile anachokikusudia. Mjasiriamali anapenda kufanya kazi yake anavyoona yeye kupitia katika mazingira yake na raslimali zinazopatikana katika mazingira husika. Daudi ni mfano wa mjasiriamali ambaye alikusudia kumuua Goliati na walipojitokeza ndugu zake pamoja na mfalme wakimpatia mbinu zao za kumshinda Goliati; Daudi alichagua kuziacha mbinu zao akaona mbinu yake aliyoitumia siku zote porini kuulia dubu na samba waliokuwa wanamwibia mifugo ingelimfaa kumuulia Goliati; alitumia mawe matano, kombeo na fimbo kumkabili na kumuua Goliati(I Samwel 17:1-58).

7. Kudhubutu kwa Angalizo.
Mjasiriamali ni mtu ambaye anaanzisha mambo na kuyasimamia na kuyasimamia mpaka atimize lengo lake bila kukata tamaa; vilevile   ni mtu anayejua kuwa kukosea anapata darasa la kujifunza na katika kutenda kuna mafanikio. Mjasiriamali mmoja asiyejulikana aliandika maneno haya kwenye mtandao wa jamii kuwa “ If FAIL you never give up because F.A.I.L means “First Attempt In LearningEND  is not end. In fact, E.N.D means “Effort Never Dies”. If you get NO as an answer , remember N.O means “ Next opportunity(Kama utashindwa usikate tamaa kwa sababu kushindwa inamaanisha Jaribio la kwanza katika kujifunza; Mwisho siyo mwisho ila ni kusema kweli Mwisho maaana yake Bidii haipotei na kama utapewa jibu la hapana kumbuka kuwa Hapana maana yake ni Fursa ya Pili.
Kuwa mjasiriamali siyo kufanya mambo bila tahadhari ila ni kudhubutu katika mchakato wa kubadili maneno kuwa kitu au kuingiza maneno katika matendo.


8. Kumiliki
Kumiliki kitu ni sifa ya ujasiriamali hata kama ni kidogo; ndiyo maana mjasiriamali yupo tayari kumiliki huduma au biashara anayoifanya hata kama ni kidogo mpaka iwe taasisi kubwa au kampuni kubwa.  Nabothi ni mfano mzuri wa Mjasiriamali aliyekataa kuuza hati miliki ya biashara yake aliposema kuwa “. . . Bwana apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu”(IWafalme 21:3).

9. Kuona mbali
Mjasiriamali anao uwezo wa kuhisi jambo linalokuja na jinsi ya kuweza kulikabili; hivyo huyu mtu anao uwezo wa kuona mbali maili nyingi zaidi ya wengine na hata anao uwezo wa kuelewa njozi ambazo mwingine amekosa tafsiri yake. Kutokana na uwezo wake wa kuona mbali anao uwezo wa kupata utatuzi wa shida au jambo kwa haraka zaidi ya watu wengine. Mfano mzuri wa Mjasiriamali kuona mbali kuliko wengine ni Yusufu aliyetafsiri ndoto ya mfalme akajikuta ameokoa Misri na kipindi cha njaa cha miaka Saba iliyokuwa mbele yao mpaka na ndugu zake Waisraeli (Wana wa Yakobo) wakaja kuponea Misri. (Mwanzo 41:14-57)

10. Kutatua tatizo kiubunifu
Mjasiriamali anao uwezo wa kutatua tatizo kwa kulifanya kuwa faida, mradi au biashara kwake na kwa jamii inayomzunguka.Hivyo anakuwa ametatua tatitizo kiubunifu. Miaka ya 2006 kuelekea 2010 nilikuwa naishi katika mji wa Arusha maeneo ya Big Y lakini ofisi zangu za kazi zilikuwa Njiro, Kijenge, na Ungaltd; Kilichonikera sana ni kuwahi ofisini asubuhi kwani mara nyingi nilikuwa natembea kwa miguu katika barabara Big Y na ile ya Philips kwenda Impala na nikagundua kuwa watu wengi nao walikuwa wanatembea kwa miguu; ndipo nilipoona kuwa kama nitakuwa natumia pikipiki ya baba mmoja aitwae Anton kunibeba nitakuwa nawahi na ndipo nilipokubaliana na rafiki yangu kuweka pikipiki za bodaboda katika keepleft ya impala na tulipata wateja wengi sana kwani tulitatua tatizo la kutembea kwa migiuu kiubunifu na huo ukawa mwanzo wa kutumia bodaboda katika mji wa Arusha.

11. Uwezo wa kujiliana.
Mjasiriamali mmoja aliandika akisema hivi A Matter of Pespective: Most problems won’t exist if people understood the difference between argument and discussion. Argument =Finding out who is right. Discussion=Finding out what is right. (Ni swala la mtazamo: Matatizo mengi yasingekuwepo Kama watu wangefahamu tofauti kati ya kushindana na kujadiliana. Kushindana=Ni kutafuta ninani sahihi. Kujadiliana = Ni kutafuta ni kipi sahihi.) Mjasiriamali ni mtaalamu wa kufanya majadiliano ili kujua kitu sahihi ili aweze kufanikisha ubunifu wake; Na kwa kuwa na uwezo wa kujadiliana inamwezesha mjasiriamali kufanikiwa katika huduma au biashara yake kwani mahusiano yanadumishwa kati ya mtoa huduma(Mjasiriamali) na wapokea huduma au wateja.

 12. Uwezo wa kuamua jambo katika hali hatarishi
Katika hali hatarishi ndiyo mazingira mazuri ya mjasiriamali anaamua mambo yake tofauti na wengine; Kwani mjasiriamali kwake ni furaha kupambana na changamoto zinazochanganya au kuogopesha wengine wengi.  Hii ni sifa juu sana ya mjasiriamali ambayo ni  Ujasiri katika kuamua na kutenda. Mtaalamu mmoja aliwahi kusema kuwa ni "afadhali kigugumizi cha kuongea kuliko kigugumizi cha kufanya maamuzi."

13. Uwezo wa kuongoza.
Mjasiriamali ni kama dreva ambaye anayo sifa ya kuendesha na huduma au biashara yake kuanzia mwanzo hadi pale atakaposhuhudia ikifanikiwa. Kazi kubwa ya mjasiriamali ni kuonyesha namna ya kufanikisha njozi zake na kusimamia kile ambacho moyoni anajua kuwa kitamfanikisha yeye na jamii inayomzunguka;Ni kwa nadra sana mjasiriamali atasimama au kukaa na kuagiza akitoa amri juu ya amri kama kiongozi yeye mara nyingi atasimama nafasi ya mwelekezaji au mwongozaji wa njia ya kufanikisha kusudi la Bisashara au huduma husika.

14. Uwezo wa Kutetea jambo. 
Professa wangu wa kozi ya Uandishi wa Andiko Utafiti (Research Paper) tukiwa darasani aliwahi kutuambia kuwa kama utaandika andiko lako unatakiwa uwe tayari kutetea kile ulichoandika kwani    ni sawa na mtoto wako;Hawezi mtu hata kama ni mwalimu wako ni vizuri ujue jinsi ya kutetea andiko lako; Ndiyo maana Katika shahada zote kuanzia ule ya uzamili na kuendelea kuna wakati wa kutetea Andiko utafiti (Defence of Research Paper) na hili linafanyika ilikuweza kueleza maana ya kile ulichofanyia utafiti.
Hivi ndivyo ilivyo kwa mjasiriamali yeyote anatakiwa awe tayari kutetea kuhusu mradi wake ili hata kama baadaye iwezekane kusaidiwa na taasisi rasmi na sisizorasmi za kifedha.

15. Kujiamini.
Kujiamini   kwa   kile  unachokifanya Mjasiriamali; Huwezi kuonyesha njia ikiwa wewe uliyetangulia hujiamini. Mjasiriamali anaamini kuwa kile anachokifanya ndicho kitu pekee katika kumfanikisha na kumwezesha kufanikisha malengo yake. Nilipopata wazo la ufugaji wa Samaki nilifanya utafiti kwa kuwasiliana na wafugaji wa Samaki nchini Tanzania ,Uganda na kupitia mtandao kuwasiliana na wakufugaji wa Samaki nchini Kenya, Korea na China; huko nilijifunza namna ya kufuga Samaki kwa njia wa mbalimbali; Nikaona nimweleze rafiki yangu mkubwa mwenye uchumi mzuri juu ya wazo hili la ufugaji wa samaki kwa kweli alinikatisha tama sana lakini kwa sababu nilikuwa nimefanya utafiti wa kutosha kuhusu njozi yenyewe sikumsikiliza ila kwenda kuingiza njozi yangu katika utendaji na kwa kweli nimeona  matokeo
ya kujiamini kama mjasiriamali.

Maoni 1 :