SOKA IGIN

WE INSPIRE AND EMPOWER FOR CHRIST'S MISSION.

Alhamisi, 29 Machi 2018

UMUHIMU WA UJASIRIAMALI KARNE YA 21



Ujasiriamali una umuhimu wa hali ya juu kwa watu wa karne ya 21 kama ifuatavyo.


Kuongeza pato
Kutokana na kuongezeka kwa ushindani wa masoko ya bidhaa au huduma fulani katika jamii mbali mbali; makampuni mengi yamekuwa yakiwaajiri watumishi ambao ni wabunifu ili kupitia ubunifu wao katika kampuni waweze kuongeza kipato. Makampuni ya simu za mikononi yamejua siri hii ndiyo maana utasikia promosheni na matangazo mbalimbali yote yakiwa na lengo la kuvuta hisia za wateja ili waweze kuongeza kipato cha kampuni.

Kubuni vitu vipya .
Ulimwengu wa karne ya 21 unatamani vitu vipya; wajasiramali wanayo ari ya kuwa tofauti na hii inawasaidia sana kubuni vitu vipya kila kunapokucha au kila baada ya Muda fulani.

Kutoa ajira
Mwalimu wa ujasiriamali akiwa anaongea na wanafunzi wake darasani aliwahi kuwaambia kuwa Mjasiriamali hatafuti ajira ila anatengeneza ajira. Binafsi nilipotafakari kauli yake nikakubaliana nayo kwani ubunifu wowote ni muhimu akiyebuni aufikishe kwenye kilele na kwa kuwa atahitaji msaada kwa vyovyote atakuwa amejiajiri na kuwaajiri wengine.

Kupunguza umaskini
Kaka Omari alifika katika mji fulani akiwa hana fedha hata kidogo akawa analalia mabox usiku kama godoro  huku  akifanya  vibarua vya kubahatisha na akagundua kuwa katika mji ule mzima hakuna mtu anayechoma mahindi; baada ya kupata kipato kidogo cha 10,000 aliamua kwenda kununua mahindi mabichi 50 kila moja kwa shilingi 100 sawa na shilingi 5000; debe la mkaa wa shilingi 3000; nauli yake na mzigo 2000. Jioni ilipofika alichukua mawe matatu akawasha moto kwenye mafiga kwani hakuwa na jiko; kwa sababu watu walikuwepo wengi eneo hilo, wakati alipoanza kumenya mahindi watu walianza kuyasubiria yaive na kwa jioni hiyo aliuza mahindi yote 50 kila mhindi kwa bei ya shilingi 500 sawa na 25,000/= kesho yake aliendelea na biashara yake hiyo akaongeza akanunua mahindi 100 na alipokuja kuyauza kila moja 500 akapata 50,000/=; Huyu Omari amekuwa kila jioni anatenga 25,000 kama akiba; kipato chake kwa mwezi kitakuwa 25,000x30=750,000/=; Kwa sasa Omari ana zaidi ya miaka mitano katika mji huo na amekuwa maarufu na kwa sasa amejenga, ameoa  na anatunza familia yake bila majuto pamoja na biashara yake. Ujasiriamali hupunguza au kufukuza umaskini kabisa.


Kupunguza Uhalifu
Baada ya biashara ya boda boda kushika kasi hapa nchini Tanzania; Rafiki yangu alipata nafasi ya kuongea na baadhi ya madreva wa boda boda kwenye mji fulani hapa nchini ambao awali walikuwa siyo watu waaminifu kutokana na tabia waliyokuwa nayo kama vile kufanya fujo mitaani; katika mazungumzo yao walipokuwa wanaongea walikiri kuwa biashara yao imewakosesha muda wa kuzurura mitaani bila lengo na kusababisha maasi. Kauli kama hizi ni Ushahidi tosha kuwa Ujasiriamali unapunguza uasi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni